Wadau wa nishati wametakiwa kuendelea kuchangia katika kuhakikisha kila kitongoji kinapata umeme katika mradi wa awamu ya tatu.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta alipokuwa akifungua kikao cha pili cha watendaji na wadau wa wakala wa nishati vijijini (REA) Wilayani Karatu.
Amesema REA wamebeba jukumu kubwa la kuhakikisha hata sekta nyingine zinaimarika kwani umeme ni hitaji kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Kimanta amesema kwa Mkoa wa Arusha una jumla ya vijiji 393 na kati ya hivyo vijiji 257 vimeshapatiwa umeme na 136 vitapatiwa umeme katika awamu ya tatu ya REA unaotarajiwa kuanza Julai 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha kila kitongoji kinapatiwa umeme ifikapo 2025.
Amesema mpaka sasa REA imejitaidi sana katika usambazaji wa umeme katika nchi nzima hivyo amewapongeza na kuwataka waongeze juhudi zaidi kwa kuhakikisha nchi nzima na maeneo yake inapata umeme.
Wakala wa nishati vijijini (REA) wamefanya kikao chao cha pili cha tathimini na mikakati ya namna ya kuboresha zaidi upatikanaji wa umeme nchini na kwa mwaka wanafanya vikao viwili vya kiutendaji.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.