Na Elinipa Lupembe
Vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa Oparesheni miaka 60 ya Muungano wametakiwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kuwa mfano kwa jamii hususani kwa vijana wenzao, kwa kuwa Taifa linawategeme.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mohamed Mkalipa, wakati akifunga mafunzo ya miezi mitatu ya Oparesheni miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika KJ833 Oljoro, na kuwataka vijana hao kwenda kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kulitumikia Taifa pamoja na kuwa mfano wa kuigwa na vijana wenzao katika jamii.
Mhe. Mkalipa licha ya kuwapongeza vijana hao, amewasisitiza kwenda kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyojifunza kwa kuonesha utofauti kati yao na vijana ambao hakushiriki mafunzo haya kwa kuonesha umahiri na uzalendo kwa Nchi yao
"Leo mmeonesha umahiri mkubwa uliotoa taswira ya jinsi wakufunzi walivyowapika, mmeonesha ukakamavu, uzalendo, utiifu na umahiri, mmeitendea haki heshima ya Amiri Jeshi Mkuu, mmeonyesha uaminifu kwake kama JKT na jeshi kwa ujumla, hivyo katumieni maarifa haya kulitumikia Taifa na sio vinginevyo" Amesisitiza Mkalipa.
Aidha, amewakumbusha wahitimu kuwa baada ya mafunzo, wanakwenda kuanza maisha ya kujitegemea kwa kutoka kwenye uangalizi wa wazazi na walimu, hivyo wako tayari kujisimamia, na kuwasisitiza kutumia vizuri uhuru wao katika kutekeleza majukumu binafsi na yale watakayopangiwa kwa kuzingatia Sheria, Kanunia na taratibu za Nchi, kwa kuepuka tabia hatarishi ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya mitandao, matumizi ya dawa za kulevya yanayoweza kuwaingiza kwenye hatia.
Hata hivyo, wahitimu hao, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu kwa vijana wa Kitanzania na kukiri kujengewa uwezo mkubwa wa kujitambua na kujithamini, kujiamini na kujitegemea, uzalendo, utiifu, uhodari na umahiri ambao utakaowawezesha kulitumikia Taifa na watanzania kwa ujumla kwa moyo wa kujitolea.
Naye Mhitimu 'Service' Salvatory Wilson Shange, amesema kuwa mafunzo hayo yamewatoa kwenye ulimwengu wa giza na kuwaleta kwenye mwanga ambao utakuwa dira ya maisha yao katika kulitumikaia Taifa la Tanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.