Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Christian Makonda amewaagiza Wakuu wa Wilaya za mkoa huo kuandaa Mpango Mkakati wa kuhamasisha Utalii katika maeneo yao.
Mhe. Makonda ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa wilaya ya Karatu, mara baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo, iliyowasilishwa na Mkuu wa wilaya Mhe. Dadi Horace Kolimba, kikao kilichofanyika kabla ya kuanza ziara kwenye wilaya hiyo.
Amesema kuwa kila halmashauri ya wilaya inatakiwa kuandaa Mpango Mkakati wa kuhamasisha Utalii ikiwa ni pamoja na kuandaa Kanzi Data (data base), itakayoonesha vivutio vya utalii vilivyopo, idadi ya hoteli na hadhi zake pamoja na maeneo ya uwekezaji yanqyopatikana kwenye halmasahuri zote ili kuwa na uelewa wa pamoja, sambamba na kurahisisha watalii wa ndani na nje ya nchi na wawekezaji kuzifahamu fursa hizo kabla ya kufika nchini.
Aidha, Mhe. Makonda amefafanua kuwa uwepo wa Kanzi Data hizo utawezesha wawekezaji na watalii kujua fursa zinazopatikana mkoani Arusha, aina ya vivutio vya utalii, kambi za utalii na hoteli zilizopo,fursa za kilimo na biashara ambazo zitawezesha kila mmoja kunufaika pamoja na kuwarahisishia wawekezaji kufanya maamuzi wakiwa kwao lakini zaidi itafungua milango ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja, mkoa na Taifa.
"Ninatamani kila mwanarusha kuufahamu Utalii vizuri na kila mmoja kwa nafasi yake kuunga mkono juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan Suluhu katika kutangaza fursa za utalii na vivutio vyake kupitia programu ya Royal Tour na Amazing iliyozinduliwa hivi karibuni nchini China, tukiufahamu Utalii tutazifahau fursa zake na kila mmoja atanufaika nazo kwa nafasi yake". Amesisitiza Mhe. Makonda
"Lazima tuwe na 'Data base' kwaajili ya wageni kujua idadi ya hoteli, kampuni za utalii aina za uwekezaji, fursa za biashara na kilimo ili wageni na wawekezaji wanaofika nchini wapate taarifa kupitia mfumo ili kuwezesha uchumi kukua" Amesema
Awali, Mhe. Kolimba amesema kuwa, wilaya hiyo ina jumla ya hoteli 74 na kambi za utalii 91 zinazosababisha wageni wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kulala Karatu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.