Watendaji wa Kata watakiwa kuwafuata wamachinga katika maeneo yao ya biashara na kuwasajiri katika mfumo wa mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na hii itawasaidia kuwatambua.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo alipokuwa akikabidhi vitambulisho 32,000 kwa Mkuu wa Wilaya ya Jiji la Arusha kwa awamu ya pili.
Amesema elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili wafahamu vigenzo na masharti ya utoaji wa vitambulisho hivyo vya Machinga, kwani bado watu wanadhani ni kila mfanyabaishara anatakiwa kupewa.
Gambo amewataka Watendaji wa Kata zote katika Jiji la Arusha kwenda kuifanya kazi hii kwa kufa na kupona na kabla ya mwezi Februari kuisha vitambulisho vyote viwe vimeshatolewa kwa wahusika.
Akipokea vitambulisho hivyo Mkuu wa Wilaya ya Jiji la Arusha Gabriel Daqarro amesema, katika ugawaji wa awamu ya kwanza Jiji la Arusha lilipata vitambulisho 8000 na vitambulisho 6719 vimeshagawiwa na 1236 bado havijagawiwa kwa wamachinga.
Ugawaji wa vitambulisho vya Machinga kwa awamu ya pili kwa Mkoa wa Arusha umepata vitambulisho 100,000 ikiwa awamu ya kwanza Mkoa ulipata vitambulisho 25,000, na ugawaji wa awamu ya pili utaendelea katika Wilaya nyingine za Mkoa huku Jiji la Arusha likipatiwa vitambulisho 32,000.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.