Na Elinipa Lupembe
Maderava Daladala, Bajaji, Bodaboda na wamiliki wa vyombo hivyo mkoani Arusha, wametakiwa kufanyakazi kwa weledi, nidhamu na uadilifu kwa kutoa huduma bora kwa wasafiri huku wakitambua umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii katika kuchangia maendeleo ya mkoa wa Arusha na Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha wakati akifungua semina elekezi kwa madereva wanaosafirisha abairia Jiji la Arusha, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Uthibiti Usafiri Ardhini - LATRA na kufanyika kwenye chuo cha ufundi Arusha.
Mhe. Mongella amewataka wasafirishaji hao kutambua kuwa wanayo dhamana na jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi ambao ni wasafiri na kuwataka kufanya kazi hiyo kwa nidhamu, weledi na umakini mkubwa kwa kuwa huduma wanayoitoa inachangia maendeleo ya mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa serikali inawategemea wasafirishaji hao, kwa kuwa kazi wanayoifanya ni sehemu muhimu, sio kazi ya kuichukulia kwa wepesi kama iilivyojengeka kuwa ni sekta ya kihuni na isiyo rasmi.
"Serikali inatambua kuwa sekta ya usafirishaji abiria ni sekta nyeti sana, hivyo msijichukulie poa, fanyeni kazi hii kwa weledi, nidhamu na uadilifu huku mkiweka kipaumbele kwenye utoaji wa huduma bora kwa wateja 'customer care' msidhani 'customer care' inafanyika benki tuu, hata ninyi mnawahudumia wateja, lazima mjithamini na kuthamini kazi yenu muhimu mnayoifanya" Amesisitiza Mhe.Mongella
Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefungua uchumi wa mkoa wa Arusha kupitia Filamu ya Royol Tour, na kusababisha ongezeko kubwa la watalii na wageni katika huo, wakipitia Jiji la Arusha na kuwataka wasafirishaji hao kujipanga kufanya shughuli zao kimkakati kuendana na hali halisi ya mkoa wa Arusha ya kuhudumia wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, watakao tumia usafiri huo wa daladala, bodaboda na bajaji.
"Kaeni mkao wa kuwahudumia wageni wa ndani na nje ya nchi, badilisheni mwelekeo wa huduma zenu, ziboresheni wekeni vyombo vyenu vya usafiri kwenye hali ya usafi na ubora, viwe na hadhi inayokidhi viwango vya kusafirisha abairia wa kigeni pia" Amesisitiza RC
Hata hivyo wasafirishaji hao, licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha, wamethibisha umuhimu wa mafunzo hayo, ambayo yamewafungua upeo kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii na katika kuchangia uchumi wa nchi na kuahidi kuwacha kuichukulia poa kazi hiyo muhimu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Daladala Arusha, Billy Albano Matewe ameweka wazi kuwa semina hiyo imewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuwajenga uelewa wa pamoja unaohusisha utoaji wa huduma bora kwa wateja, ushirikiano wa sekta ya usafirishaji na sekta nyingine ikiwemo serikali na mamalaka za serikali.
"Kutoka na mafunzo haya pamoja na makubaliano yaliyofanyika baada ya serikali kuingilia kati na kutatua changamoto zilizokuwa zinatukabilia maafisa wasafirishaji, tukuahidi mkuu wa mkoa hakuta kuwa na mgomo tena, kwa kuwa tayari tumetambua umuhimu wa sekta hii na madhara ya mgomo kwa kijamii na kiuchumi" Amesema
Mwenyekiti wa Bajaji Arusha Abdulrazak Khalifa Malya, ameishukuru na kuipongeza serikali kwa kutambua na kuthamini kazi wanayoifanya na kuahidi kuendelea kushirikiana na Mamlaka za serikali katika kuboresha sekta hiyo ya usafirishaji wa abiria jijini Arusha.
Aidha amempongeza Mhe. Mongela kwa mkakati wa Jiji la Arusha wa kupanga bajaji hizo katika vituo rasmi jambo ambalo limeondoa mgogoro uliokiwepo baina yao na maderava daladala uliosababisha mgomo miezi miwili iliyopita.
Naye Mwenyekiti wa Bodaboda Jiji la Arusha, Okero Costantine, amemuomba mkuu wa mkoa wa Arusha kuwaunganisha madereva bodaboda wa mkoa mzima ili waweze kuzungumza lugha moja kutokana na ongezeko la vijana wanaojishughulisha na bodaboda mkoani humo, kundi ambalo linahitaji kushirikishwaji ili kuimarisha sekta hiyo kwa maendeleo ya taifa.
Awali mafunzo hayo ya siku moja yamewakutanisha vyama vya wasafirishaji Daladala, Bajaji, bodaboda pamoja na wamiliki ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya usalama na umuhimu wa huduma wanazozitoa kwa jamiii na kwa maendeleo ya taifa.
#arushafursalukuki
#KaziInaendelea
PICHA ZA KIKAO KAAI
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.