“Mkasome kwa makini kanuni za uchaguzi wa mwaka 2019 na kufuata ratiba vizuri ya uchaguzi kwa kuzingatia mipaka ya ramani ya uchaguzi kwenye maeneo yenu”.
Akitoa maagizo hayo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) injinia Joseph Muhanga, katika kuapishwa kwa wasimamizi saba wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Mkoa wa Arusha.
Pia, ameitaka sekretarieti ya Mkoa na ofisi za wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia kwa umakini maandalizi na uchaguzi wote wa serikali za mitaa,unaotarajia kufanyika mapema Novemba mwaka huu.
Baada ya kushuhudia kuapishwa kwa wasimamizi hao Injinia Muhanga alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa umma kutoka sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Jiji la Arusha na Halmashauri ya Arusha kwa lengo la kujitambulisha baada ya uteuzi wake.
Amesisitiza usimamizi mzuri wa fedha za miradi inayotolewa na serikali na kuwataka wakurugenzi kuhakikisha wanazisimamia kwa umakini na miradi yake inatekelezeka katika kiwango bora.
Ameupongeza uwongozi wa Mkoa pamoja na halamshauri zake katika kufanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya elimu na kusimamia vizuri miradi mbalimbali katika Mkoa.
Mapema mwezi huu Waziri Ofisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mhe. Seleman Jaffo alifanya uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kwa mwaka 2019 takribani 184 kwa nchi nzima na Mkoa wa Arusha umepata wasimamizi saba wa kusimamia halmashauri zote saba.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.