Kundi la Watalii maarufu wa kupanda milima mirefu Duniani kutoka nchini China, wamewasili mkoani Arusha na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. John V.K Mongella, na
kufanya mazungumzo pamoja na kushiriki chakula cha jioni, hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha, jioni ya leo tarehe 26 Desemba, 2023.
Kundi hilo likiwa na jumla ya Watalii 54, likongozwa na Ndugu. Xia Boyu, wako nchini kwa ajili ya kushiriki Tamasha la Kupanda Mlima Kilimanjaro, lililoandaliwa na Kampuni ya kitanzania ya Gosheni Safaris.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapokea watalii hao, Mhe. Mongella ameeleza kuwa, ujio wa wageni hao umetokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi ya Tanzania na China, uhusiano ambao ulitengenezwa na waasisi wa mataifa hayo na kuendelezwa na viongozi waliopo sasa.
“Nichukue fursa hii kuwakaribisha Tanzania, kushiriki Tamasha la Kupanda Mlima Kilimanjaro, ukiwa ndio msimu mzuri wa kupanda mlima Kilimanjaro, ninaamini mtafurahia muonekano na mandari nzuri ya mlima huo mrefu Afrika" Amesema Mhe. Mongella.
Aidha ameipongeza Kampuni utalii ya Goshen safaris, kwa kundaa Tamasha hilo, ambalo ni muhimu na lenye manufaa kwa nchi ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo China.
Amefafanua kuwa, msimu wa mwisho wa mwaka, ni msimu mzuri zaidi kwa kupanda mlima Kilimanjaro, hali itakayowafanya kufurahia mandari nzuri ya mlima na kuweza kuitangaza Tanzania kupitia mlima huo wa Kilimanjaro
Katika hafla, hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa licha ya kuwakaribisha watalii hao, amewapatia vyeti ya kuwapongeza wapanda mlima hao maarufu dunia,ambao wamekwishapanda mlima mrefu zaidi duniani Everest Zaidi ya mara 10.
Naye Kiongozi wa Watalii hao, Xia Boyu, amekiri kufurahishwa na uwepo wao nchini pamoja na kuvutiwa na mandhari nzuri ya mkoa wa Arusha, huku akiamini safari yao ya siku 10 itakuwa nzuri na ya furaha kwa wote.
"Tumefurahi kuwa Tanzania, Tanzania ni nchi nzuri, watu wake ni wazuri wana upendo, safari yetu itakuwa nzuri na ya furaha, tunafuhia kupanda Mlima Kilimanjaro lakini tunafurahi zaidi kushiriki Tamasha hili kubwa" Amesema Boyu
Awali, Wageni hao wapo nchini kwa siku 10, wakitumia siku 7 kupanda mlima Kilimanjaro na siku 3 kwaajili ya safari, huku Kundi likiwa ni maarufu duniani kwa kupanda mlima Mrefu zaidi, wakiwa tayari wamepanda mlima Everest zaidi ya mara 10, mlima ambao ni wa kwanza kwa urefu duniani.
Ikumbukwe kuwa, ujio wa watalii hao ni matokea ya Filamu ya Royal Tour, iliyochezwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasaan, ikiwa ni mkakati wa kutangaza utalii ndani ja nje ya nchi.
#Arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.