Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, amewaagiza Maofisa Watendaji wa Kata zote za Mkoa wa Arusha kufahamu bajeti ya mapato na matumizi ya Kata husika kwa mwaka mzima.
Mhe. Makonda ametoa agizo hilo wakati akisikiliza kero na changamoto za wananchi wa Kata ya Mateves, kufuatia agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi la kumtaka kurudi kata ya Mateves ili kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi hao, ambapo Mhe. Makonda amerudi leo mapema Juni 04, 2024.
Mhe. Makonda amewaagiza Maofisa hao kuhakikisha wanazifahamu vema bajeti na mipango ya kata zao kwa mwaka husika pamoja na utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kwenye kata husika huku wakifahamu muda wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Amefafanua kuwa, kila Mtendaji anatakiwa kufahamu aina ya miradi iliyotekelezwa kwenye kata husika na gharama zake kisekta huku mikataba ya miradi hiyo, kiasi cha fedha alicholipwa mkandarasi na wazabuni waliotekeleza miradi, idadi ya wanufaika wa miradi hiyo pamoja na tija ya miradi kwa wanufaika.
"Ninakerwa na uwajibikaji na ufanisi mdogo wa baadhi wa watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji, baadhi yao wamekosa sifa za kuwatumikia wananchi kutokana na uwajibikaji mdogo kwenye vituo vyao vya kazi, unaosababisha kero na malalamiko mengi kwa wananchi na kuichukia Serikali" Amebainisha Mhe.Makonda.
Hata hivyo Mhe. Makonda ameahidi kuanza kufanya ziara ya kata kwa kata mkoani Arusha na kuwataka Maofisa hao wa kata kujiandaa kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli wa maendeleo za kata zao wakati wa ziara hiyo maalum ya kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi.
#ArushaNaUtalii
#kaziinaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.