@ortamisemi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa @mohamed_mchengerwa amewataka wauguzi kula kiapo cha utoaji wa huduma bora.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo jijini Tanga wakati wa kufungua Kongamano la kisayansi na Mkutano Mkuu wa 51 wa Chama Cha Wauguzi Tanzania.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshamaliza jukumu la kujenga miundombinu, kuweka vifaa tiba, kununua, vitendanishi na kuajiri watumishi na kuwa kilichobakia huduma bora kwa wananachi.
« Mpaka sasa tuna miundombinu bora na kila kitu kinachotakiwa kwenye utoaji wa huduma lakini huduma bado ni mbovu, hamna kauli nzuri na wananchi wanalalamika, kwa kweli hili linanikosesha raha. »
« Tukifanikiwa kwenye kutoa huduma bora tutakua tumepiga hatua kubwa sana kwenye sekta ya afya, » amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza: « sasa msiondoke hapa mpaka mle kiapo cha kutoa huduma bora kwa niaba ya wauguzi wengine wote walioko kwenye vituo vya kutolea huduma na mkakitendee haki kiapo kwa kufanyakazi kwa moyo na kwa mapenzi yote kwa watanzania. »
Amesema wagonjwa wanapokuja hospitalini wanahitaji faraja na msaada wa saikolojia kwa kupokelewa vizuri na kupewa maneno mazuri anaanza kupata nafuu.
« Lakini wengine wenu hawana kauli nzuri, hawawasikilizi wagonjwa mpaka wapewe fedha hii sio afya, kwa taaluma yenu nataka niwaone mkila kiapo cha utoaji wa huduma bora. »
Aidha, Waziri Mchengerwa alimuekeza Katibu Mkuu - TAMISEMI kuhakikisha anafanyia kazi changamoto za wauguzi zilizowasilishwa ikiwemo ile ya muundo kwa wauguzi na upandaji wa madaraja.
« Haiwezekani watu mfanyekazi ya kujitoa halafu hata madaraja hampandishwi, hii si sawa sasa naelekeza changamoto hii ifanyiwekazi na mwakani tutakapokutana tena iwe imeshafanyiwa kazi. »
Awali akiwasilisha taarifa ya Wauguzi hao Katibu Mkuu wa chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Samson Mwangoka amesema wauguzi wana changamoto ya kutopandishwa madaraja, muundo usiotoa kipaumbele kwa taaluma na kutokuwa na bajeti.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.