Wazazi watakiwa kuwa makini na udanganyifu hasa katika kipindi cha kufanya uhamisho wa watoto wao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020.
Yamesemwa hayo na katibu tawala wa Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega alipokuwa akitangaza rasmi uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2020 kwa mkoa wa Arusha.
“Kuna watu wanatabia ya kuwadanganya wazazi watawasaidia kupata shule wanazoziitaji kirahisi kwa ajili ya watoto wao, lakini ukweli na taratibu zilizopo ni, mzazi mwenyewe ndio anatakiwa kuanzia katika ngazi ya shule aliyopangiwa mtoto wake kisha atapatiwa kibari katika ngazi ya halmashauri”,alisema Kwitega.
Amesisitiza zaidi kama uhamisho ni wa shule zilizopo ndani ya halmashauri basi mzazi haitaji kufika katika ngazi ya Mkoa ila kama niwakutoka halmashauri moja kwenda nyingine ndio mzazi atatakiwa kumalizia hatua zote katika ngazi ya Mkoa.
Kwitega amewataka wazazi pia kusubiri mpaka shule zikifunguliwa na wanafunzi wote wamewasili mashuleni ndio taratibu za uhamisho zianze kwani kwa kufanya hivyo itasaidia halmashauri husika kufahamu shule gani zina upungufu na zipi zimejitosheleza.
Akitoa taarifa ya ufaulu wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza afisa elimu Mkoa wa Arusha bwana Halifan Masukila, amesema jumla ya wanafunzi 37,655 ndio waliofanya mtihani kwa mwaka 2019 na kati yao wanafunzi 34,509 ndio walifaulu sawa na asilimia 91.67.
Ambapo wakiume walikuwa 16,573 na wakike 16,636 na hivyo kufanya idadi kubwa ya watahiniwa wa kike kufanya vizuri zaidi ya watahiniwa wa kiume.
Bwana Masuka amesema ufaulu kwa mkoa wa Arusha umepanda ukilinganisha na mwaka jana ambapo ufauli ulikuwa wa asilimia 87.30 na kuufanya Mkoa kushika nafasi ya pili kitaifa ikiufuatia mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mwaka 2020 jumla ya wanafunzi 29,770 wameshapangiwa shule kwa ajili ya masomo yatakayoonza mapema Januari 2020 na wanafunzi 4,739 wamepangiwa shule lakini wanasubiri ukamilifu wa miundo mbinu katika shule hizo hasa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
Hivyo amewataka wazazi kuwa nasubira hasa kwa wale wanafunzi wanaosubiri ujenzi wa miundombuni kikamilika katika shule walizopangiwa.
Mkoa wa Arusha unaendelea kufanya vizuri zaidi katika sekta ya elimu na hii inatokana na utaratibu uliowekwa na uongozi wa Mkoa wa kuhakikisha elimu inakuwa kwa kasi sana ikiwemo ufanyaji wa mtihani mmoja kwa shule zote za Mkoa na hii inasaidia kuweza kupima kiwango cha ufundishaji kwa walimu na kuwapa motisha zaidi pale wanapofanya vizuri.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.