WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaaga viongozi wa dini 104 ambao wanaelekea Dodoma kwa treni ya mwendokasi (SGR) kwenda kushiriki ibada maalum ya kuliombea Taifa inayotarajiwa kufanyika kesho, Jumatatu, Aprili 22, 2024.
Treni hiyo imeondoka stesheni ya Dar es Salaam saa 8.53 mchana ikiwa na viongozi hao, waandishi wa habari, waimbaji wa nyimbo za injili na kaswida, viongozi wastaafu wa Serikali, watendaji wa Shirika la Reli nchini, wawakilishi wa ubalozi na watedaji wengine wa Serikali.
Amewaaga viongozi hao na watendaji wengine wa Serikali na taasisi mbalimbali leo (Jumapili, Aprili 21, 2024) kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye stesheni ya Tanzanite, barabara ya Sokoine, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na viongozi hao kabla ya kupata dua ya kuombea safari yao, Waziri Mkuu amesema: “Leo ni siku muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Tuko kwenye wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na tunashuhudia safari ya kwanza ya treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.”
Amesema Tanzania inathamini dini na kutoa uhuru wa wananchi wake kokote na ndiyo maana amani, utulivu na mshikamano vinakuwepo nchini. “Tanzania ni nchi iliyoteuliwa na Mungu kwa utulivu wake, amani na uvumilivu.”
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.