Na Mwandishi wetu
Kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya Kiwanda cha Elia Food kilichopo Wilayani Longido, mkoani Arusha kutokupata malighafi kwa ajili ya kuchakata nyama, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amefika Wilayani humo na kukutana na wafanyabiashara wa mifugo pamoja na Uongozi wa Kiwanda hicho kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.
Akiongea katika mkutano ambao ulihusisha uongozi wa Mkoa, muwekezaji wa kiwanda hicho na wafanyabiashara wa mifugo uliofanyika wilayani humo Novemba 16, 2023, Waziri Ulega aliwaeleza kuwa lengo la kukutana nao ni kutaka kujua kwanini wafanyabiashara hao wa mifugo hawaendi kuuza mifugo yao katika kiwanda hicho na badala yake wanakwenda kuiuza nchi jirani.
Baada ya kusikiliza maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara ya kwanini hawaendi kuuza mifugo yao katika kiwanda hicho, Waziri Ulega aliamua kuchukua hatua kadhaa za kusuluhisha mgogoro huo.
Hatua ya kwanza aliyoichukua ameelekeza iundwe timu ya Wataalam itakayokuwa chini ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wa Mkoa na wananchi wazoefu wa biashara ya mifugo ili kutafuta majawabu ya kutatua changamoto hizo ndani ya wiki mbili na kuwasilisha taarifa kwake.
Aidha, katika kikao hicho alimuagiza Afisa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuhakikisha wanafungua tawi la benki hiyo Mkoani Arusha ili iwe rahisi kwa wafanyabiashara ya mifugo kupata mitaji kwa urahisi.
Halikadhalika, Waziri Ulega aliutaka uongozi wa Kiwanda hicho kuachana na tabia ya kuwakopa wafanyabiashara ya mifugo kwani kwa kufanya hivyo kunapelekea wafanyabiashara hao kutafuta sehemu ambapo wanauza mifugo yao bila kukopwa.
Awali, wakati wakitoa maoni yao, Wafanyabiashara hao walisema kuwa changamoto kubwa inayowafanya wasipeleke mifugo yao katika kiwanda hicho ni kubadilika badilika kwa bei, biashara kufanyika kwa mkopo na kukosekana kwa uwazi wakati wa kupima uzito wa mifugo.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Kiwanda cha Elia Food, Bw. Shabbir Virjee aliishukuru Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kibali cha kuuza ngozi nje ya nchi na kusema kuwa biashara hiyo inaenda vizuri.
Aidha, alibainisha kuwa pamoja na biashara hiyo ya ngozi kwenda vizuri hata hivyo kuna changamoto ya ubora kutokana na baadhi ya ngozi hizo kuchorwa alama kubwa na wafugaji.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.