Na Daniel Gitaro
Zaidi ya wananchi laki 1.9 Mkoani Arusha, wamepata elimu kuhusu masuala ya sheria pamoja na msaada wa kisheria bila gharama na wengine kwa gharama kidogo, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kuanzia 24 -30 Januari, 2024 na kuhitimishwa Februari 01, 2024.
Akizungumza wakati wa kilele cha Siku ya Sheria Tanzania, sherehe iliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Joachim Tiganga amesema kuwa, idadi hiyo ya wananchi imefikiwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo vyombo vya habari na kuonana ana kwa ana, huku watu 516 kati ya hao wakipatiwa msaada wa kisheria.
"Katika wiki hiyo, watu wenhi zaidi walijitokeza huku Sheria mbalimbali zikifundishwa, kutokana na idadi ya watu, tuliowahudumi mwaka huu, tumevunja rekodi ya miaka iliyopita kwenye maadhimisho kama haya". Amesema Mhe. Tiganga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella amesema kuwa, Taasisi zinazojihusisha na Haki Jinai zinapaswa kutambua namna bora ya kuunganisha mifumo yao katika kuboresha kazi na kuleta tija na Muunganiko unaoweza kufanywa kwa kutumia TEHAMA na kuwa na manufaa zaidi kwa jamii zetu.
Hata hivyo Mhe. Mongella ameongeza kuwa, dhima ya siku ya sheria inamlenga mwananchi na wadau wa sheria kwa ujumla wake kuendana na kasi ya Mahakama ya Mtandao ambayo ndiyo dira ya Mahakama kwa sasa pamoja na kutambua na kuelewa mifumo mbalimbali iliyowekwa katika upatikanaji na utoaji haki jinai.
"Wananchi wana nafasi kubwa zaidi ya kujitafutia kwanza taarifa muhimu kuhusu haki zao zinazopatikana katika Tovuti za Taasisi za Umma kwa kuwa Silaha bora ya kupigania Haki ni kuelewa upatikanaji wa hiyo Haki unayopigania ipo chini ya Sheria, Kanuni au Taratibu ipi". Amesisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Chapter ya Arusha, Wakili George Njooka, amesema kuwa kila Mtanzania mpenda haki anawajibu wa kuunga mkono na kuhakikisha kuwa nia njema, utashi na juhudi za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha na kuboresha mifumo Taasisi na Taasisi za Haki Jinai Nchini zinatekelezwa kwa tija na ufanisi mkubwa.
"Sisi kama chama cha wanasheria nchini, tunauhakikishia Umma kuwa tumejidhatiti kimkakati ili kuhakikisha kwamba tunatoa mchango wa kitaalam kwa kadri itakavyohitajika ili kutekeleza kwa tija na ufanisi mkubwa mapendekezo yaliyotolewa ya tume ya haki jinai". Ameweka wazi.
Awali, Maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka 2024 yamebeba Kauli mbiu ya "Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa; Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai"
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.