Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amesema zoezi la sensa halina itikadi ya kisiasa, hivyo kila mtu ana wajibu wa kushiriki na kuhamasisha wengine.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini, Siasa, Kimila na watendaji wa vitongoji na vijiji wa Halmashauri ya Arusha katika kikao cha kuhamasisha zoezi la sensa.
" Zoezi la sensa halina itikadi ya kisiasa,niwaombe kila mmoja ashiriki kuhesabiwa na kuhamasisha wengine kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia, Jamii na Taifa kwa ujumla".
Maendeleo hayaitaji siasa kwani ni kwa ajili ya kila mtanzania katika itikadi za kisiasa tofauti, hivyo tuungane kwa pamoja kuweza kulifanikisha hili.
Amewataka viongozi hao wakatoe elimu kwa wananchi hasa zoezi la sensa sio la siku moja bali ni siku 6 kaunzia Agosti 23 hadi 29 na usiku wa Agosti 22 kuamkia 23 sensa itaanza kwa wale wasio na makazi maalumu kama vile wasafiri.
Aidha, Mhe. Mongella amesema atakae husika kukwamisha zoezi hili ajue sheria itachukua mkondo wake bila kuonea yeyote.
Pia, Mongella amewataka wananchi wa kata ya Oljoro kuhakikisha siku ya tarehe 23 hadi tarehe 29 Agosti wanaacha taarifa zao majumbani ili iwe rahisi kwa karani wa sensa anapopita kuzipata kwa urahisi.
Amewataka wakawe mabalozi wa zoezi zima la sensa ili Serikali inapoleta huduma mbalimbali kwa wananchi kila mmoja aweze kunufaika.
Mhe. Mongella pamoja na Katibu Tawala bwana Missaile Musa wanaendelea na ziara ya kuhamasisha wananchi wajitokeze katika zoezi la sensa kwenye kila halmashauri ya Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.