Zoezi la kupisha ujenzi wa barabara ya Mianzini hadi Ngaramtoni kwa kubomoa nyumba zote zilizopo ndani ya mita 10 kila upande mwisho wake ni Disemba 26,2022.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara hiyo katika halmashauri ya Jiji la Arusha na Arusha.
" Serikali imeshaleta fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii, haiwezekani ikacheleweshwa na watu wachache wasiotaka kubomoa nyumba zao",alisema.
Aidha, ameitaka Wakala wa barabara Tanzania (TANROAD) kuendelea kutoa elimu ya sheria ya barabara kwa wananchi ili waweze kuifahamu vizuri na kujenga uelewa wa pamoja.
Mongella amesema kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007 upana wa barabara ulitakiwa kuwa mita 20 kila upande lakini serikali ya Rais Samia inayowajali wananchi wake na haitaki wapate kero hivyo imepunguza na kuwa mita 10 kwa kila upande.
Amewataka wananchi wa maeneo ambayo barabara hiyo inapita, kuunga Mkono juhudi hizo za serikali kwani barabara inaleta maendeleo.
Pia, amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya ajira wakati ujenzi huo ukiendelea.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha Muhandisi Regnand Massawe amesema barabara hiyo ya Mianzini Sambasha ina urefu wa KM 12 na ile inayoanzia Olemringaringa hadi Ngaramtoni ina urefu wa KM 6.
Amesema barabara hiyo kwa ujumla ina urefu wa KM 18 na itagharimu Bilioni 22 hadi kukamilika kwake na kwa sasa ujenzi umefikia 8%.
Matarajio ya kukamilika kwa mradi huo ni mwaka Agosti 2023 ikiwa umeanza Agosti 2022.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa yakukagua ujenzi wa barabara ya Mianzini hadi Ngaramtoni ilikuwa kwa lengo la kukagua ujenzi na kusikiliza changamoto za wananchi wa maeneo hayo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.