Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewataka viongozi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha fedha za lishe wanazozitenga zinafanya kazi za lishe pekee.
Ameyasema hayo kwenye kikao cha tathimini cha lishe Mkoa wa Arusha.
Halmashauri nyingi zimeonesha kutekeleza afua ya utoaji fedha kwa watoto chini ya miaka 5 lakini changamoto ni uhakika wa fedha hizo kutumika katika kazi husika.
"Viongozi wa Halmashauri hakikisheni na mkasimamie fedha za lishe kwa umakini hasa kwa matumizi yaliyopagwa, itakuwa haina maana Halmashauri ipate asilimia 100 ya utoaji fedha wakati hazijawafikia walengwa", alisema.
RC Mongella, amesisitiza kuwa utoaji wa fedha hizo uwe wa mapema zaidi kuliko kusubiria mwisho wa mwaka ndio Halmashauri inazitoa zote, kwani kwa muda huo inakuwa vigumu kwenda kutekeleza kazi husika.
Swala la ufuatiliaji wa fedha hizo liwe jukumu la kila mtu ili tuweze kupata matokea mazuri zaidi.
Aidha, amesema swala la lishe ni nyeti na ili lifanikiwe inabidi lifanywe kwenye shughuli za kila siku.
Nae, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha bwana Missaile Musa amezitaka halmashauri za Mkoa wa Arusha kufuta rangi ya njano na nyekundu katika kadi ya kupimia afua za lishe.
Amesema kwa kufanya hivyo hali ya lishe Mkoa itapanda zaidi.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Silvia Mamkwe amesema yeye na timu yake wataenda kusimamia sekta ya lishe kwa umakini zaidi ili kuweza kupunguza kiwango cha udumavu kwa kiasi kikubwa katika Mkoa.
Afisa lishe Mkoa wa Arusha Bi. Rose Mauya, ametoa msisitizo wa Halmashauri kuhakikisha zinatenga fedha za lishe kutokana na uhalisia ili iwe rahisi kutekelezeka
Kikao cha nusu ya pili cha tathimini ya lishe kwa Mkoa wa Arusha kwa Mwaka 2021/2022 kimefanyika kikiwa kimejumuisha wakuu wa Wilaya, wakurugenzi na wataalamu mbalimbali kutoka ngazi ya Mkoa, Wilaya, Halmashauri na taasisi binafsi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa