Uongozi wa Halmashauri ya Arusha umepongezwa kwa kupata hati safi kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa miaka mitano mfululizo.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Serikali za Mitaa, Mkoa wa Arusha,Bi. Susan Mnafe kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Dkt. Athumani Kihamia, wakati wa kikao cha kamati ya Fedha Utawala na Mipango, cha kupitia Hoja za Ukaguzi wa Hesabu za halmashauri ya Arusha kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Licha ya kutoa pongezi hizo, Bi. Susan ametoa maelekezo kwa uongozi wa halmasahuri hiyo, kuhakikisha kabrasha la hoja hizo linafuata muundo na miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI pamoja na kujaza majedwali hayo kilingana na maelekezo.
Aidha amesisitiza kuweka majibu ya hoja, yakiwa na viambatanisho visivyosababisha maswali, huku hoja nyingine zikiainisha wazi mikakati ya utekelazaji wake, zikionyesha dhahiri kiasi cha fedha kinachohitajika, idadi ya shughuli zitakazotekelezwa kwa mwaka pamoja na muda halisi wa utekelezaji.
Hata hivyo, Suzan amewasisitiza wataalam hao, kuhakikisha wanatoa mikopo isiyo na riba kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sambamba na kufuatilia fedha hizo kurejeshwa kwa wakati kwa kuwa wakurugenzi wote, hupimwa kutokana na uwajibikaji wa mikopo hiyo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Naye, Mkaguzi Mkazi Mkoa wa Arusha, Honest Muya, amewataka wataalamu hao, kuwasilisha majibu ya hoja hizo, kulingana na ushauri uliotolewa na wataalamu kwa kushirikiana na waheshimiwa madiwani ili hoja hizo ziweze kufutwa kabla ya mkutano wa Baraza la Madiwani.
Hata hivyo Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Mheshimiwa Ojung'u Salekwa, amewshukuru wataalamu na waheshimiwa madiwani kwa ushirikiano wao, unaowezesha halmashauri kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo,na kuwata wataalamu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo ya serikali, pamoja na kuwasisitiza wataalamu hao, kupokea ushauri uliotolewa na Mkaguzi Mkazi sambamba na kuwasilisha majibu yenye tija ili kufuta hoja zisizo za lazima.
Aidha amemuomba Katibu Tawala kupeleka kilio kikubwa cha halmashauri cha upungufu wa wataalamu hasa katika sekta ya Afya, upungufu unaosababisha baadhi ya zahanati kukamilika majengo na vifaa lakini kushindwa kufunguliwa kutokana na kukosekana kwa wataalamu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa