Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kutokuwa na hofu ya kuondolewa katika maeneo ya hifadhi.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani na wadau wa hifadhi wilayani Ngorongoro.
Lengo kubwa la kikao hicho ni kuona namna bora ya kutunza uhifadhi wa misitu na wanyama katika eneo hilo.
Mhe. Majaliwa amewataka wananchi wa Ngorongoro kupuuzia maneno yanayozungumzwa mitaa kwani hayana ukweli wowote wa kuondoa wananchi katika maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro na pori tengefu.
Akisisitiza zaidi Mhe Mjaliwa amesema Serikali haiwezi kuonea mtu yoyote kwani watu wote niwatanzania na wala haibagui kabila na hata dini.
Wajibu wa Serikali ni kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitatua kwani ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.
Msisitizo wa Serikali nikuona namna ya kuhifadhi tunu za wanyama na misitu kwa kuzitunza na mslahi mapana ya nchi.
Nae, mbunge wa wilaya ya Ngorongoro Emmanuel Shangai amesema wananchi wa wilaya hiyo wapo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ili kufikia Suluhu ya migogoro hiyo.
Kiongozi wa kimila ( Laigwanani) bwana Joel Kremesi akizungumza kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo amemshukuru Waziri Mkuu kwa kutambua kuwa wananchi hao niwahifadhi wazuri wa wanyama na misitu.
Bwana Kremesi amesema wao wapo tayari kujadili hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha maamuzi yanapatikana kwa pande zote mbili kushiriki kikamilifu.
Mhe.Waziri Mkuu amefanya kikao hicho na wadau wa hifadhi ikiwa ni kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mhe.Rais Samia Suluhu yakukutana na wadau hao na kutafuta muafaka.
Kikao hicho kilijumuisha viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, Naibu mawaziri, makatibu wakuu, viongozi wa chama, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, madiwani na wenyeviti wa Wilaya hiyo ya Ngorongoro.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa