Na Elinipa Lupembe
Watumishi halmashauri ya Ngorongoro, wametakiwa kuongeza bidii katika kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi, kwa kuwa Serikali imewawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi, kwa kujenga Jengo la kiasa la Halmashauri hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha, Loy Thomas Ole Sabaya, mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala Halmashauri ya Ngorongoro, mradi unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 3, na tayari jengo hilo limeanza kutumiwa na watumishi hao.
Mwenyekiti Sabaya ameweka wazi kuwa, Serikali ya awamu ya sita imefanya mabadiliko makubwa katika sekta zote, kwa kutekeleza miradi ya maendeleo nchi nzima,miradi inayowagusa watanzania wote, na kusisitiza kuwa miradi hiyo, imewafikia takribani wakazi wote wa Ngorongoro, wakiwemo watumishi wa Serikali.
Amewapongeza watumishi hao, kwa kujitoa kufanya kazi na kuweka wazi kuwa, Serikali imewekeza fedha nyingi kujenga jengo hilo, ikiwa na mategemeo makubwa kutoka kwa watalamu wa halmashauri ya kutoa huduma bora kwa wananchi zinazokwenda sambamba na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Ngorongoro.
"Ngorongoro ya sasa sio ile ya zamani tunayoifahamu, yapo mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo, mabadiliko ambayo na nyinyi watumishi mnahusika katika kuibadilisha Ngorongoro, tumieni jengo hili kurejesha fadhila kwa Serikali ya kuwahudumia wananchi, Serikali ina matarajio makubwa kutoka kwenu" Amesema Mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri hiyo, Nassor Shemzigwa, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Jemadari Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazingira bora na salama kwa watumishi na kuahidi kuwasimamia watalamu wote, kuongeza kasi ya kufanya kazi, ya kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi kisekta ili kufikia malengo ya Serikali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa