Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Kimanta amewataka madereva wote wa mkoa wa Arusha kuzingatia sheria za barabarani pindi wanapokuwa wanaendesha vyombo nya moto.
Amezungumza hayo alipofanya kikao na viongozi wa chama cha wasafirishaji cha mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA), mapema ofisini kwake.
Amewata katika kutekeleza majukumu yao waweke mazoea ya kujenga mahusiano mazuri na wote wanaofanya nao kazi zikiwemo taasis mbalimbali za serikali.
Amesema mahusiano mazuri yatawasaidia kufanya kazi kwa urahisi bila kuwa na changamoto nyingi na hata zikitokea wanashirikiana kuzitatua kwa haraka zaidi.
Amesisitiza zaidi atakuwa bega kwa bega na viongozi hao kwa kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati.
Katibu wa umoja wa madereva wa mabasi makubwa bwana Simon Ntakune, amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo wao kama madereva ni vituo vingi vya askari wa barabarani,ambavyo vinapelekea kupoteza muda mrefu kwa kusimamishwa mara kwa mara.
Pia, wameomba uongozi wa mkoa kufanya marekebisho ya kituo cha mabasi madogo (daladala) cha Kilombelo ambacho kina mashimo makubwa kwenye baadhi ya maeneo na hivyo kupelekea usumbufu kwa magari.
Mheshimiwa Kimanta amekuwa akikutana na makundi mbalimbali ya wadau waliopo katika Mkoa wa Arusha kwa lengo la kujitambulisha kwao kama kiongozi wa Mkoa na pia kuweza kufahama changamoto zao kama wananchi wa mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa