_Usanifu wakamilika, yatarajiwa kukuza utalii na uchumi wa Arusha_
Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza rasmi utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Mto wa Mbu- Engaruka, Engaruka- Ngaresero ili kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo Utalii na Uwekezaji, barabara itakayoziunganisha Wilaya za Monduli na Ngorongoro.
Akizungumza na Viongozi wa dini, Mila na Serikali pamoja na Watendaji kuanzia ngazi ya Kitongoji Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, leo Jumatano Septemba 10, 2025 wakati akihitimisha ziara yake Wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amesema usanifu wa barabara hiyo ya Mto wa Mbu- Engaruka- Ngaresero yenye urefu wa Kilomita 74 umekamilika na hatua za kumpata Mkandarasi zimeshaanza.
"Lengo la Mhe. Rais na serikali yake ya awamu ya sita ni kutatua hili tatizo la muda mrefu na kuunganisha Wilaya za Monduli na Ngorongoro suala ambalo litavutia zaidi uwekezaji unaofanywa kwenye kiwanda cha Magadi soda Engaruka katika Wilaya ya Monduli pamoja na kutimiza dhamira njema ya kukuza utalii Mkoani Arusha kupitia Ziwa Natroni lililopo Wilaya ya Ngorongoro, Wana Monduli Mhe. Rais anatupenda sana." Amesema Mhe. CPA Makalla.
Aidha CPA Makalla amefafanua kuwa barabara hiyo itajengwa kwa vipande vitatu ambavyo ni Kilomita 23 za Mto wa Mbu- Selela, Kilomita 27 za Selela- Engaruka pamoja na Kilomita 24 za Engaruka- Ngaresero, akiwataka Viongozi wa Wilaya hizo kusimamia kikamilifu mradi huo pamoja na miradi mingine inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na katika ubora uliokusudiwa.
Kadhalika CPA Makalla licha ya kuahidi kusimamia na kusukuma uharaka katika utekelezaji wa mradi huo, ameweka wazi kuwa Dkt. Samia ametoa shilingi Bilioni 17 kwaajili ya utekelezaji wa mradi wa skimu ya Umwagiliaji Wilayani Monduli, mradi ambao kukamilika kwake utanufaisha Vijiji zaidi ya kumi na moja, akisema Mkandarasi wa kutekeleza mradi huo tayari amepatikana na kazi itaanza hivi karibuni.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa