Imeelezwa kuwa, Serikali ya awamu ya sita imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu mkoa wa Arusha, kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 267 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za elimu pamoja na ujenzi wa miundombinu ya shule.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Albano Musa, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.CPA Amos Makalla @amosmakalla, kwenye Kongamano la Wadau wa Elimu kuelekea Juma la Elimu Mkoa wa huo, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo leo Septemba 17,2025.
Katibu Tawala Missaile amesema kuwa, mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita, katika sekta ya elimu yamechagizwa na juhudi, uwajibijikaji na weledi wa walimu, ambao ndio wasimamizi wa shughuli zote za elimu shuleni ikiwemo usimamizi wa ujenzi wa miundombinu yote inayofanyika shuleni.
Ameweka wazi kuwa, kwa miaka minne ya Dkt.Samia Mkoa wa Arusha umepokea shilingi Bilioni 267 huku Bilioni 107.08 zikitumika kwenye uboreshaji wa miundombinu ya shule, miradi ambayo imefanya mapinduzi makubwa kwenye shule za sekomdari na msingi ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya wanafunzi na kupandisha kiwango cha taaluma shuleni.
"Niwahakikishie licha ya walimu kusimamia taaluma shuleni, wameweza pia kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye shule zao, ninawapongeza sana kwa kazi kubwa, iliyoleta heshima kwa Serikali yetu, niwasihi walimu kubadilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia, jiwekeeni mipango ya kujiendeleza kimasomo ili muendane na wakati, fanyeni kazi kwa bidii na weledi ili kufikia malengo ya Serikali". Amesema Missaile
Hata hivyo walimu wa Mkoa wa Arusha, hawakuwa nyuma kuipongeza Serikali, kwa kuboresha miundombinu ya shule, jambo ambalo licha ya kuongeza ari ya wanafunzi kusoma inawapa urahisi walimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi.
Mwenyekiti wa TAHOSA Mkoa wa Arusha Mwl. Omari Nyangu amesema kuwa, maboresho katika sekta ya elimu yamewaondolea wazazi adha ya kuchangia ujenzi wa madarasa jambo ambalo limeongeza hamasa ya wazazi kupeleka watoto shule.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa