Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo kufufua kitengo cha kudhibiti mimea ili kiweze kusimamia majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika nchi.
Ameyasema hayo alipokuwa akikagua eneo lililovamiwa na Nzige katika kata ya Engaruka wilayani Monduli.
Amesema kufufuliwa kwa Kitengo hicho kutasaidia kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Nzige,ambayo kwa sasa yanaendelea vizuri na baadhi ya maeneo Nzige wameisha.
“Wananchi toeni taarifa pindi mkiona nzige katika maeneo yenu, ili serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti.”
Majaliwa amesisitiza ushirikiano uwendelee katika kupambana na janga la Nzige hasa na nchi jirani.
Akitoa taarifa ya hali ya mapambao ya Nzige katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema, Nzige kwa mara ya kwanza waliingia nchini katika wilaya ya Simanjiro na wakadhibitiwa wote na mara ya pili waliingia wilayani Longido.
Kwa sasa wilaya za Simanjiro, Siha na Mwanga Nzige wamedhibitiwa wote na katika Wilaya ya Longido tathimini itatolewa ili kufahamu kama Nzige hao wameisha au bado pia nae neo la Engaruka.
Profesa Mkenda amesema zoezi la kupambana na Nzige limeenda vizuri kwasababu kulikuwa na ushirikiano mziuri sana baina ya Serikali, wananchi na hata nchi Rafiki kama Zambia, Uganda na Zimbabwe.
Amesema zoezi kubwa lilipo kwa sasa ni wataalamu wanaendelea kufuatilia yale maeneo ambayo Nzige wanahisiwa waloitaga mayai ili waweze kuyaangamiza kabla hayajakomaa na kutoa Nzige wapya.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Kimanta Pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mgwira wamesema zoezi la kuwaangamiza Nzige katika Mikoa yao limekuwa rahisi kwasababu wananchi wametoa ushirikiano mkubwa sana hasa kwa kutoa taarifa pale wanapohisi kuna uvamizi wa Nzige katika maeneo yao.
Mhe. Majaliwa ameridhishwa na namna zoezi la kupambana na Nzige lilivyofanyka katika Mikoa hiyo mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara na amewata wataalamu kuendelea kufuatilia uvamizi huo wa Nzige katika maeneo mbalimbali ya Nchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa