Watalam kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha tayari wameanza rasmi ujenzi wa nyumba ya kuishi yenye vyumba vitatu na sebule mama wa miaka 70, Bibi Penina Petro mkazi wa Kijiji cha Siwandete Kata ya Kiranyi wilayani Arumeru, kufuatia ahadi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Paul Christian Makonda wakati wa program ya Oparesheni rejesha Haki iliyofanyika wiki iliyopita.
Mhe. Mkuu wa mkoa aliahidi kumjenga nyumba Bibi huyo wakati wa kliniki yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Arusha na ndipo bibi huyo alipoanza kulia na kueleza masaibu ya nyumba yake kudondoka na ndugu zake kugoma kumjengea nyumba hiyo, kutokana na kutojaliwa kupata mtoto na hivyo kudai kuwa hakuna haja kwa madai bibi huyo hana muda mrefu wa kuendelea kuishi duniani.
Tayari wataalamu wa ujenzi wamefika kwenye eneo la bibi huyo kwaajili ya upembuzi wa awali na kupima eneo hilo na kulingana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ujenzi wa nyumba hiyo unatarajiwa kuanza wiki hii.
Katibu Tawala Msaidizi Ujenzi, Mkoa wa Arusha, Mhandisi Makange, amefika kwenye eneo la bibi huyo na kuanza hatua za ujenzi wa nyumba hiyo ya kisasa yenye vyumba vitatu na sebule.
Hata hivyo,Bibi Penina ametumia fursa hiyo kumuombea kheri na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wanyonge na kuwa majibu ya changamoto zao huku pia akimshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda kwa kuja na kliniki ya kuwasikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuwa na nidhamu katika kuahidi na kutekeleza.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa