Waziri ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa mheshimiwa Selemani Jafo amezitaka wilaya zote nchini kuanza mara moja ujenzi wa hospitali za wilaya.
Ameyasema hayo alipotembelea hospitali ya Longido na Eworendeke wilayani Longido mkoani Arusha na kufurahishwa na ujenzi unavyoendelea.
“Serikali kwa sasa imeshatoa milioni 500 za ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Longido na mpaka ikamilike itaitaji kiasi cha shilingi bilioni 1.5, hivyo kwa fedha hizo zinatosha kuanza ujenzi”, alisema.
Amesema amefurahishwa sana na ujenzi wa hospitali zote katika mkoa wa Arusha kwa kiwango kikubwa na ameshawishika kuona hata pia ujenzi wa hospitali za wilaya utakuwa mzuri.
Ameagiza hadi kufikia Novemba 14, 2018, ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Longido uwe umeshaanza kwa kufuata mchoro wa ramani uliotolewa na TAMISEMI ili hospitali zote za wilaya nchini ziwe na mfanano.
Aidha, amewahasa wahandisi kuhakikisha wanasimamia ujenzi kwa umakini kwani amebaini baadhi yao hukaa maofisini mda mwingi badala ya kwenda kusimamia ujenzi.
Ameziagiza wilaya zote nchini kufikia Novemba 30, 2018 majengo yote yawe yamekamilika ili kuruhusu huduma za afya kuanza mara moja.
Nae Afisa Mtendaji kata ya Kimokouwa Victa Kabati, amesema kituo cha afya cha Eworendeke kitakuwa msaada mkubwa sana kwa kutoa huduma ya afya kwa wananchi wa kata hiyo na eneo la Namanga kwa ujumla.
Wananchi wengi wa kata hiyo wamekuwa wakipata shida ya kupata huduma za afya na kuwalazimu kwenda hadi nchi ya jirani, lakini kwa kukamilika kwa kituo hicho wengi watakuwa wamesogezewa huduma karibu na kuondoa usumbufu wa kuzitafuta katika umbali mrefu.
Akitoa pongezi kwa serikali ya wilaya mwenyekiti wa kamati ya ujezi John Shinabaki, amesema ujenzi umeenda vizuri kwa kiasi kikubwa kwani fedha zilikuwa zinapatikana kwa wakati.
Amewataka wananchi wa kata ya Kimokouwa kushirikiana bega kwa bega na viongozi wa wilaya ili ujenzi ukamilike haraka na duhuma zianze kutolewa.
Waziri Jafo amefanya ziara ya siku moja mkoani Arusha katika wilaya ya Londigo kwa kukagua hospitali mbili za Longido na Eworendeke na kupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kusimamia ujenzi mzuri wa hospitali katika wilaya zote na kuzitaka wilaya nyingine kuiga mfano huo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa