Katibu Tawala masaidizi,utawala na Rasilimali watu Mkoa wa Arusha Bwana David Lyamongi amezita kamati za kutoka huduma za Maji ngazi ya jamii kusimamia kikamilifu ukusanyaji na matumizi ya fedha za Maji.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha wadau na vyombo vya watoa huduma ya Maji ngazi ya jamii kwa Mkoa wa Arusha kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia.
Kamati hizo ziliundwa baada ya Serikali kuona kuna umuhimu wa kuwa na vyombo vya kusimamia miradi ya Maji ambayo serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha na miradi hiyo mingi huaribika na mingine kutokamilika.
Hivyo Serikali ilipofika mwaka 2019 ikaona kuna umuhimu wa kuanzisha kamati hizo kwa kila halmashauri ili ziweze kusimamia miradi hiyo kwa karibu na kuilinda ili iendelee kutoa Maji.
Pia, amezitaka kamati hizo kufuata Sheria na taratibu za utoaji huduma za Maji ili kuwarahisishia wao kuweza kuwafikia wananchi wengi na kwa urahisi.
Sambamba na hayo amezitaka kamati hizo kuendelea kulinda vyanzo vya Maji katika maeneo yao dhidi ya uchepushaji wa Maji unaofanywa na wakulima, wafugaji , pia ukataji miti hovyo na uchafuzi wa vyanzo vya Maji.
Kwa kufanya hivyo vyanzo vingi vya Maji vitaweza kutoa Maji ya kutosha kwa wananchi.
Kamati hizo pia zinatakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa kutumia Maji salama, kupima Maji na kupata taarifa sahihi za Maji.
Aidha, amesema Serikali imejiwekea mkakati ifikapo mwaka 2025 utoaji wa Maji vijijini ufikie asilimia 85.
Nae, Meneja wa Wakala wa Maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Arusha Mhandisi Emmanuel Makaidi, amesema lengo kubwa la kikao kazi hicho ni kujengeana uwelewa wa pamoja kuhusu namna ya utoaji huduma nzuri za Maji.
Pia kuweza kuzifahamu changamoto za wadau hao na vyombo hivyo ili Serikali ikishirikiana na wadau ione namna ya kuzitatua na kuweka mazingira rahisi ya upatikanaji wa Maji kwa wananchi.
Amesema hadi sasa Serikali imetoa fedha nyingi katika miradi ya Maji kwa awamu tatu, ya kwanza Bilioni 600 ziliwekwa kwenye bajeti ya RUWASA na awamu ya pili Bilioni 207 ziliongezwa na awamu ya tatu, zaidi ya Bilioni 3.5 zimetolewa kutoka mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano ya UVIKO 19.
Amesisitiza kuwa changamoto za kamati hizo ni muda sasa wakuzigeuza kuwa fursa ili kuweza kuboresha zaidi usimamizi wa miradi hiyo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa