Na Elinipa Lupembe.
Maafisa Rasilimali watu afrika wamekumbushwa kuwa, uongozi wa rasilimali watu katika sekta ya Umma ni zaidi ya kuajiri na kusimamia watumishi ni kwenda mbali zaidi kwa kianda mazingira wezeshi kwa wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kukuza uwezo wao, kuvumbua, na kuleta mabadiliko chanya katika utendaki kazi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Festo Shemu Kiswaga, wakati akitoa salamu za Mkoa wa Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Paul Christian Makonda kwenye Mkutano wa 9 wa Mtandao wa Mameneja na Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika sekta za Umma Barani Afrika 2024, unaofanyika mkoani Arusha kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) mapema leo Novemba 04, 2024.
Amesema kuwa, viongozi wetu wa rasilimali watu wanapaswa kuwa na mbinu za kisasa zinazojumuisha maarifa, uadilifu, na ufanisi katika kujenga watumishi wanaoweza kustahimili na kubadilika na changamoto zinazokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya kiuchumi kwenye nchi za Afrika.
Aidha, amewakaribisha washiriki na wageni wote, Arusha kwa kuwahakikishia usalama wao na kuwa mkoa unajivunia kuwa wenyeji wa mkutano huo muhimu wenye lengo la kuimarisha uongozi na utawala bora, pamoja na uvumbuzi katika sekta ya Umma.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alivyowekeza nguvu na fedha nyingi katika sekta ya Utumishi na amekua mfano bora kwa watumishi wa Umma, wanalipwa mishahara kwa wakati, wanapandishwa madaraja, wanapewa nafasi za kujiendeleza kimasomo pale inapohitaji jambo linalochochea watumishi kufanyakazi kwa bidii na kusukuma mbele gurudumu la amendeleo nchini" Ameweka wazi Mhe.Kiswaga
Kauli mbiu ya mkutano huo ni "Utawala Stahimilivu na Ubunifu; Kutunza Sekta ya Umma Ijayo Kupitia Uongozi wa Rasilimali Watu"
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa