Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mh. Marco Ngumbi, amemkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha wilayani Longido alipofika kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kumpa taarifa fupi ya wilaya hiyo, mapema leo Mei 23, 2024 kwenye Ofisi za Mkuu wa wilaya hiyo.
Mhe. Ng'umbi licha ya kuwakaribisha wageni wote wakiongozwa na Mhe.Makonda ameweka wazi kuwa, hali ya Usalama wilaya ya Longido ni shwari huku wananchi wote kwenye vitongoji 176, vijiji 50, kata 18 na Tarafa 4, wakiendelea na shughuli zao za kila siku za kijamii na kiuchumi.
Amesema kuwa, kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali ya awamu ya sita huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa kwa aliyoifanya kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 44, fedha ambazo zimetekeleza miradi katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, mifugo, umeme ambapo vijiji vyote 49 tayari vimefikiwa na umeme na awamu ya pili ambayo imeanza kupelekea kwenye vitongoji.
Hata hivyo mkuu wa wilaya hiyo, amemueleza Mhe.Makonda kuwa, katika ziara yake atatembelea jumla ya miradi mitatu yenye thamani ya shilingi Bilioni 17.1 na kuitaja miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji Sinya, ujenzi wa nyumba ya watumishi zahanati ya Leremeta, mradi wa shule mpya ya Sekondari ya wasicha Samia pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye Mkutano wa Hadhara utakaofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Namanga.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa