"Hakikisheni mikopo mnayokopeshwa mnarudisha tena kwa wakati,hii itasaidia kujijengea imani yakuweza kukopeshwa tena".
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akikabidhi hundi ya mikopo kwa vikundi vya kina Mama, Vijana na wenye Ulemavu Wilayani Karatu.
Amevitaka vikundi vilivyopata Mkopo kwenda kutumia fedha hizo kwa tija ili na wengine waweze kuona faida ya mikopo hiyo.
Aidha, ameziagiza halmashauri zote kufanya tathimini za Mikopo hiyo ya 10% katika uhalisia wa maendeleo hususani kwenye miradi iliyoanzishwa na vikundi hivyo.
Ameipongeza halmashauri kwa kusimamia marejesho ya mikopo iliyosaidia kuongeza kiwango cha mikopo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Karatu Karia Rajabu amesema halmashauri hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza naya pili mwaka 2022/2023 wametoa fedha kiasi cha Milioni 4.8 kwa vikundi 482 vya wamama, Vijana na wenye Ulemavu.
Bwana Karia amevitaka vikindi vilivyokopeshwa wauchukulie Mkopo huo kama dhamana na warudishe ili kila mtu aweze kunufaika nao.
Mratibu wa mfuko huo kutoka halmashauri ya Karatu Bi. Adelida Shauri amesema mikopo hiyo kwa miaka ya nyuma ilikuwa inarudishwa kwa riba lakini ilipofikia mwaka 2018/2019 riba iliondolewa.
Amesema, kwa mwaka 2022/2023 vikundi vilivyopatiwa mkopo huo ni 60 vyenye wanawake 441, vikundi 7 vyenye vijana 35 na vikundi 6 vya watu wenye ulemavu 6.
Kutokana na usimamizi mahili walioufanya katika marejesho kumeiwezasha halmashauri ya Karatu kuweza kutumia marejesho hayo kuwakopesha wengine pamoja na mapato ya ndani.
Halmashauri ya Karatu imeweza kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato iliyopelekea kuongezeka kwa 10% ya mikopo ambapo Milioni 408 zilizotolewa, Milioni 280 ni mapato ya ndani na Milioni 180 ni marejesho ya mikopo ya nyuma.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa