Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amemwagiza Afisa Elimu Mkoa bwana Halfan Omari Masukira kumvua madara ya ukuu wa shule mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Irkaswa bwana Arbogastus Mushi na mwalimu wa taaluma kwa kushindwa kusimamia ufundishaji katika shule hiyo iliyopo Wilayani Longido.
Maelekezo hayo ameyatoa alipokuwa akizungumza katika kikao na Maafisa Elimu kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.
Kimanta amesema ni aibu kubwa sana kwa mwalimu mkuu kutohakikisha vipindi vyote vinafundishwa na walimu wake kwa wakati.
“Hii inaashiria ni usimamizi mbovu wa mwalimu mkuu na mwalimu wa taaluma, kwani wanafunzi wamekuwa wakifundishwa masomo machache kwa siku huku mwalimu mkuu hajui chochote”, alisema.
Amewataka maafisa elimu hao kwenda kuwasimamia walimu wakuu wa shule kwa ukaribu zaidi, kwani Mkoa wa Arusha unasifa ya kushika nafasi nzuri katika matokea ya mitihani mbalimbali, hivyo baadhi ya walimu wakuu wasikwamishe jitihada hizo.
Nae, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha bwana David Lyimongi, amemuagiza Afisa Elimu mkoa bwana Masukira kuhakikisha miongozo yote inayoletwa kutoka TAMISEMI iwe inaendana na uhalisia wa hali ya sasa ili sekta ya elimu iendelee kuimarika zaidi.
Mkoa wa Arusha umekuwa ukifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa na kwa mwaka 2020 kidato cha sita Mkoa ulishika nafasi ya 7 Kitaifa, kidato cha nne nafasi ya 1, kidato cha pili nafasi ya 1, darasa la saba nafasi ya 2 na darasa la nne nafasi ya 3.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa