Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na sekta binafsi kuongeza juhudi katika kujenga usawa wa kijinsia na wanawake katika uongozi na ngazi nyingine za maamuzi.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua jukwaa la uongozi wa vijana kwa mwaka 2021 kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jijini Arusha.
Amesema jukumu hilo nila kila mtu la kuhakikisha usawa wa kijinsia na wanawake unaimarika hasa katika siasa na uongozi.
Kwa upande wa Tanzania tayari hatua mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo uteuzi wa Majaji wanawake takribani 13 kati ya 28 wa Mahakama kuu sawa na asilimia 43 na Makatibu Tawala wa Mikoa wanawake walikuwa 12 kati ya 26 sawa na asilimia 46.
Mhe.Majaliwa amesema juhudi hizi zimefanywa na Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe.Samia Suluhu.
Amefafanua zaidi kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya wanawake umoja wa Mataifa ya mwaka 2017 inaonesha kuwa itachukua miaka 50 kufikia usawa wa kijinsia katika ushiriki wa siasa na miaka 118 katika usawa wa malipo duniani kote.
Nae, Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki amewahakikishia vijana hao mawazo yao waliyoyatoa atayawasilisha kwa watunga sera wa Jumuiya hiyo ili yaweze kutoa muelekeo madhubuti kwa Vijana katika maswala ya Kijinsia.
Aidha, amewataka viongozi wa sasa kuendelea kuwafundisha na kuwashirikisha vijana ili kuwajenga zaidi katika siasa na waweze kuwa viongozi bora.
Jukwaa la uongozi wa vijana kwa mwaka 2021 limefanyika Jijini Arusha kwa siku 3 ukiwa na agenda ya bara la Afrika lijalo litakuwa na kutengeneza ajira, makazi na uwezo wa kulisha mabara machanga ulimwenguni.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa