Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kudhihirisha mapenzi yake kwa wakazi wa Arusha mara baada ya kuagiza dawa nyingine za binadamu kwaajili ya Kliniki ya Matibabu inayoratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda @baba_keagan
Akizungumza na wananchi waliojitokeza siku ya nne ya kambi ya Matibabu wa Madaktari Bingwa na Mabingwa Wabobezi Arusha, inayoendelea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid mapema leo, Juni 27, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema kuwa, Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha mapenzi yake kwa wananchi wa Arusha, hasa wale hali ya chini wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu, ameagiza dawa nyingine kwa ajili ya wagonjwa watakaohudhuria kiliniki hii.
Mhe. Makonda ameelezea kuwa, jumla ya watoto 10 wamebainika kuwa na matatizo kwenye mfumo wa uzazi, ambapo Hospitali ya Taifa Muhimbili imejitolea kuwafanyia upasuaji wa bure ili kurejesha mifumo yao ya uzazi (Korodani) katika hali yake ya kawaida.
Hata hivyo, Mhe. Makonda amewashukuru wadau wote, wanaoendelea kujitolea vitenganishi na vifaa mbalimbali vya matibabu akiwemo Mtumishi wa Mungu Mtume Boniface Mwamposa wa Kanisa la Arise and Shine (Inuka Uangaze) aliyejitolea vitimwendo 15, kwaajili ya kuwasaidia Wazee na watu wenye ulemavu wa miguu akisema malengo ya kambi hiyo ni kuwa na viti 1000.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa