Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla @amosmakalla leo Jumamosi Septemba 20, 2025 ametembelea na Kukagua utekelezaji wa mradi wa maboresho na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Lake Manyara Wilayani Karatu, akisisitiza umuhimu wa ukamilisha wa mradi huo katika viwango, ubora na muda waliokubaliana kwenye Mkataba ili kuchochea shughuli za usafiri, uchumi na Utalii kupitia Uwanja huo wa ndege.
Uwanja wa ndege wa Lake Manyara unaboreshwa kwa kuongezwa njia za kuruka na kutua ndege na kuwa na upana wa Mita 30 na urefu wa Mita 1500 kutoka upana wa mita 21 na urefu wa mita 1220 za sasa, ukigharimu takribani shilingi 88, 539, 522.550 na ukitekelezwa na Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Company.
Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na miundombinu ya Maegesho ya ndege, maegesho ya magari na barabara za kuingia na kutoka kiwanjani hapo, usanikishaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, kujenga uzio, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege pamoja na ujenzi wa jengo la uchunguzi wa hali ya hewa.
Kulingana na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe amesema kukamilika kwa maboresho hayo kutaongeza usalama na uwezo mkubwa wa kubeba na kupokea ndege kubwa aina ya ATR 42 yenye uwezo wa kubeba abiria 72 na pia utasaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Karatu pamoja na pato la Mkoa wa Arusha kwa Ujumla.
Kulingana na wasimamizi wa mradi huo, hadi sasa mkandarasi amekabidhiwa eneo la mradi na anaendelea na maandalizi, Mhandisi Mshauri akiendelea na mapitio ya usanifu wa kina wa uwanja wa ndege pamoja na kazi zilizoongezeka kwenye mradi ikiwa ni ujenzi wa daraja la Mto Athumani lenye urefu wa Mita 60 kwenye barabara ya Mto wa Mbu- Loliondo pamoja na Kalavati la midomo mitatu eneo la Manyara Kibaoni, barabara ya Makuyuni- Ngorongoro Mkoani Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa