Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, ameagiza kukamilika haraka kwa ujenzi wa jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege wa Arusha eneo la Kisongo, kabla ya Septemba01,2024 ili liweze kutoa huduma kwa abiria wanaotumia uwanja huo.
Mhe. Makonda ametoa agizo hilo, alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo la abiria mapema leo Agosti 16, 2024, jengo lenye uwezo wa kuhudumia takribani abiria 1000 kwa wakati, ukilinganisha na jengo la zamani lililokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 150 pekee.
"Shauku yetu sisi wananchi wa Mkoa wa Arusha ni kuhakikisha uwanja wetu unafanya kazi kwa saa 24 na wale wenye ndege zao binafsi waweze kutumia uwanja huu, ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye lengo lake ni kuufungua mji wa Arusha na kuongeza hamasa ya watalii kuja nchini mwetu." amesema Mhe. Makonda.
Hata hivyo, Mhe. Makonda ameagiza kutumika kwa teknolojia katika utoaji wa huduma kwa abiria wanaotumia uwanja huo pamoja na kuweka miundombinu ya kutangaza utalii wa Arusha, ili kuvutia zaidi watalii wanaofika Mkoani hapa kuweza kutembelea vivutio vinavyopatikana na mkoani Arusha na mikoa ya pembezoni.
Naye Meneja Kiwanja hicho, amsema Kiwanja hicho ni miongoni mwa viwanja vyenye miruko mingi ya ndege nchini ikilinganishwa na viwanja vingine hivyo Upanuzi wa kiwanja hicho utafikia lengo na mahitaji ya abiria.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa