Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametembelea na kukagua utoaji wa huduma kwenye jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Arusha, na kuagiza Uongozi wa uwanja huo kukamilisha haraka upatikanaji wa baadhi ya huduma ambazo bado hazipatikani uwanjani hapo.
Mhe. Makonda amekagua utoaji wa huduma hizo leo Septemba 27, 2024 ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza kutumika kwa jengo hilo ambapo alipata pia nafasi ya kuzungumza na watalii na wageni wanaotumia uwanja huo ambao wengi wao wamesifu uboreshaji mkubwa na uharaka katika huduma zinazotolewa uwanjani hapo.
Mhe. Paul Christian Makonda pia amewataka watoa huduma mbalimbali katika uwanja huo kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma bora kwa watumiaji wa kiwanja hicho, akisisitiza umuhimu wa huduma bora na za kisasa uwanjani hapo kama sehemu ya kuchagiza na kuwafanya watalii na wageni mbalimbali kurudi mkoani Arusha.
Kwa Upande wake Bw. Godfrey Kaaya, Meneja wa uwanja wa Arusha amesema jengo hilo la abiria limekamilika kwa asilimia 98, akimuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa kufikia Disemba mwaka huu, huduma zote zitakuwa zinapatikana ndani ya Jengo hilo jipya na la kisasa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa