Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, amekutana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, kujadili maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani leo tarehe 10 Februari, 2025.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye `Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa, viongozi hao wamekubaliana kuweka msisitizo mkubwa katika michezo kama sehemu ya kuadhimisha siku hiyo muhimu ikiwemo kuandaa mashindano ya mpira wa miguu kwa wanawake, ambapo timu nne za wanawake zitashiriki, zikiwemo Simba Queens, Yanga Queens, JKT Queens na Fountain Gate FC.
Aidha, Viongozi hao wamekubaliana kawa, TFF itaweka banda maalum katika maadhimisho hayo ili kutoa elimu kuhusu maendeleo ya soka la wanawake na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo mbalimbali.
Mbali na michezo, maadhimisho hayo yataambatana na Wiki ya Utoaji wa Huduma kwa Wanawake, ambapo sekta mbalimbali zinazohusiana na maendeleo ya wanawake zitashiriki kutoa huduma na elimu kwa wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani.
Hata hivyo, Mhe. Paul Makonda amesisitiza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuinua hadhi ya mwanamke katika nyanja mbalimbali, hususan michezo, afya, elimu na uchumi na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana kwa karibu kuhakikisha hafla hiyo inafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, ameahidi kuwa shirikisho hilo litaendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka la wanawake na kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha mpira wa miguu kwa wanawake unapata msukumo unaostahili.
Maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea, na wananchi wa Arusha wanatarajiwa kushiriki kwa wingi katika hafla hiyo ambayo itaadhimishwa Kitaifa 08 Machi, 2025 Mkoani Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa