Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella,ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), Kituo cha afya Levolosi, Jiji la Arusha ikiwa ni ziara yake ya kawaida ya kikazi leo 21 Desemba, 2023.
Akikagua maendeleo ya mradi huo, ambao mpaka sasa jengo liko hatua ya msingi na kufikia asilimia 22 ya ujenzi, Mhe. Mongella, ameagiza uongozi wa Jiji la Arusha, kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo hilo ili liweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, ambalo ndilo lengo la Serikali.
Amweka wazi kuwa, lengo la Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao, na ndio sababu ya kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi, hususani huduma za afya kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya huduma za afya nchini.
"Kama Serikali imeshatoa fedha za mradi, ni jukumu letu watalamu kuhakikisja mradi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha, wananchi wanahitaji huduma, tusiwacheleweshe kupata huduma, simamieni ujenzi ukamilike". Amesema Mhe. Mongella
Akisoma taarifa ya Mradi, Mhandisi wa Ujenzi, Jiji la Arusha, Mhandisi Jacob Mwakyambiki, amesema kuwa, mradi huo wa jengo la OPD Kituo cha Afya Levolosi, utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.2 mradi ambao umefikia asilimia 22 ya utekelezaji wake na unategemea kukamilika ifikapo mwezi Aprili 2024.
Amefafanua kuwa, mradi utahusisha jengo hilo lenye sakafu mbili (horofa mbili) sakafu ya chini, ikiwa na Idara ya ushauri wa madaktari, idara ya mionzi yenye huduma za Xray na Utra sound, idara ya Dawa, maabara na Min theatre,
Ameongeza kuwa, sakafu ya kwanza, ikijumuisha idara ya meno, macho, ushauri wa madaktari, huku sakafu ya pili ikiwa na wodi ya wanawake, wanaume, watoto pamoja na vyumba na ofisi za watumishi
Mkuu wa Mkoa wa Arusha amefanya ziara ya kukagua hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo jiji la Arusha katika sekta ya afya, elimu na uwekezaji.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa