Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya Msingi Korongoni kata ya Lemara, Jiji la Arusha, ikiwa ni maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi, kwa mwaka wa masomo unaotarajia kuanza Januari, 2024.
Mhe. Mongella amewaagiza viongozi na wasimamizi wa mradi huo, kuongeza kasi ya ujenzi, ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.
Akiwasilisha Taarifa ya mradi huo, Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Korongoni, Mwl. Itika Kirango amesema kuwa, mradi huo, unategemea kutekelezwa wa gharama ya shilingi milioni 765, ambapo utekelezaji wake unafanyika kwa awamu, kadri fedha zinavyopatikana kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, ukijumuisha ujenzi wa jengo la ghorofa.
Aidha, awamu ya kwanza utekelezaji imefanyika kwa mwaka wa fedha 2022/2023, kwa kujenga msingi wa jengo la ghorofa sakafu ya chini yenye vyumba 4 vya madarasa na matundu ya vyoo 11 kwenye sakafu ya kwanza, kwa gharama ya shilingi milioni 365.
Awamu ya pili ya ujenzi, imegharimu shilingi milioni 400, ambazo zinaendeleza ujenzi kwa sakafu ya kwanza na ya pili, inayojumuisha vyumba 8 vya madarasa na matundu ya vyoo 22, mradi unaotekelezwa kwa fedha za mwaka wa fedha 2023/24.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa