@ortamisemi
Serikali imefanya marekebisho mbalimbali kwenye sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za mitaa sura 290 kupitia sheria ya Fedha namba 2 ya mwaka 2023.
Mabadiliko hayo yameweka jukumu la kusimamia na kukusanya Kodi ya Majengo pamoja na ushuru wa mabango kwa mamlaka za serikali za Mitaa ili kuziongezea wigo wa mapato mamlaka hizo.
Maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI leo Juni 19, 2024 wamewajengea uwezo wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga pamoja na Watendaji wa Kata na Vijiji namna ya kukusanya kodi ya majengo ambapo mafunzo haya yamelenga kutekeleza mabadiriko ya Sheria ya fedha na miongozo mbalimbali kwa lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zote nchini.
Wakati akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Ndg. Kulanga Kanyanga amesema uwepo wa mafunzo hayo ni hatua nzuri ya Serikali kwa Halmashauri, kwani ukusanyaji wa mapato hayo utaleta tija kwa Jamii, kuimarisha uratibu wa shughuli mbalimbali za Halmashauri pamoja na Taifa kwa ujumla.
« Ndugu Wataalam na Watendaji, sisi ni miongoni mwa Halmashauri 47 zilizoteuliwa kupata mafunzo ya kujengewa uwezo wa kutumia mfumo wa TAUSI katika kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya majengo ambapo itawezesha kuleta maendeleo makubwa kwa Halmashauri na Jamii yetu, tunaishukuru sana Serikali yetu » alisisitiza Ndg. Kanyanga
Aidha, baada ya mafunzo hayo Halmashauri inapaswa kuanza kukusanya kodi ya majengo, pia kutoa vibali vya ujenzi na vya matangazo kwa njia ya mtandao ambapo mteja ataweza kujihudumia mwenyewe kupitia dirisha la Mlipakodi (TAUSI Taxpayer Portal).
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa