Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda amezitaka Taasisi za Ulinzi Arusha kushirikiana na waandishi wa habari ili wapate taarifa muhimu kuhusu Taasisi zao na mambo yanayoendelea kwenye Taasisi hizo.
Mhe. Makonda amesema hayo, kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi za Ulinzi mkoa wa Arusha, ikiwepo Jeshi la Polisi, TAKUKURU,Jeshi la Zimamoto, Uhamiaji, Taasisi ya kupambana na Dawa za Kulevya, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo, Julai, 11,2024.
Amefafanua kuwa upo umuhimu wa taasisi hizo, kushirikiana na waandishi wa habari, kwa kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu taasisi zao na mambo yanayoendelea kuliko kusubiri kuona taarifa kwenye vyomba vya habari, taarifa ambazo hazina uhalisia.
Uchumi wa mkoa wa Arusha, unategemea sana ujio wa watalii kutoka ndani na nje ya nchi, uwepo wa taarifa zisizo na uhalisia licha ya kuharibu taswira ya mkoa, zinaharibu taswira ya nchi sambamba na kuharibu soko la utalii, soko ambalo ni tegemeo la mkoa na Taifa.
"Ninatamani wakuu wa Taasisi za Ulinzi kuwa na mahusiano mazuri na waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa kuwapa taarifa, ili kuwa na uelewa wa pamoja utakaowezesha wananchi kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi, hali hii itaondoa taharuki za mara kwa mara". Amesisitiza Mhe. Makonda.
Zipo taarifa ambazo zinatolewa na vyombo vya habari, taarifa ambazo hazina uhalisia na kusababisha taharuki kwa wananchi na wageni, upo umuhimu wa kuwa na vyanzo sahihi vya taarifa za mkoa wa Arusha, taarifa ambazo zitajenga heshima ya mkoa na Taifa kwa ujumla wake.
"Ili kuondoa taarifa zinazozua taharuki na sintofahamu kwa wananchi, ni muhimu kuwa na utaratibu wa kuwapa taarifa sahihi wanahabari, wananchi watapata taarifa sahihi, hivyo ni vema vyombo vya usalama vikatoka taarifa kwa uŕahisi ili wananchi wazifahamu, zaidi zitauletea sifa ya mkoa wetu, mkoa ambao una wageni wengi wa ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amewataka waandishi wa habari kuweka uzalendo mbele kabla ya kutoa habari jambo ambalo litaweka utaifa mbele badala ya maslahi binafsi.
"Ni muhimu vyombo vya habari kuweka maslahi ya Taifa mbele, hakuna maana ya kulipaka matope Taifa letu kwa 'interest' za muda mfupi, tuangalie uwepo wa vita ya kiuchumi duniani" Amesema Kamanda Masejo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa