Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amewataka Watanzania kudumisha amani na mshikamano kama tunu ya taifa.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo kijiji cha Esilalei Wilayani Monduli wakati wa ukaguzi wa mradi wa maji kwenye ziara yake ya siku nne anayoifanya wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha ambapo ameeleza kuwa mafanikio mengi yaliyofikiwa nchini ni matokeo ya amani na utulivu vilivyodumu kwa miaka mingi.
Amesisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa huku akileta maendeleo yasiyoangalia dini, kabila wala chama cha siasa kama vile wa miundombinu ya barabara, miradi ya maji, umeme na shule, huduma ambazo zinawagusa wananchi wote na ni kiashiria cha mshikamano wa kitaifa unaopaswa kulindwa.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuzingatia sifa na uwezo wa viongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa unaotarajia kufanyika mwaka huu badala ya kushawishiwa na zawadi ndogondogo ili kuchagua kiongozi na kusisitiza kuwa kiongozi bora ni yule anayechaguliwa kwa misingi ya uwezo wake wa kuleta maendeleo, si ahadi au upendeleo wa muda mfupi.
Mradi huo wa maji ambao umekamilika awamu ya kwanza utagharimu kiasi cha sh, bilioni 1.9 ambao utahudumia wananchi 8,757 kutoka vijiji vya Eslalei, Losirwa na makao mapya.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa