Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewaaidi wananchi wa Mkoa huo kutumia fursa zilizopo hususani kwenye Viwanda, Kilimo na Ufugaji ili kuleta maendeleo ya Mkoa.
Ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye hafla ya kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya ya Ngorongoro na Arusha, katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
RC Mongella amesisitiza kuwa ili maendeleo yapatikane ni lazima kuwe na Utumishi uliotukuka, amani na mshikamano baina ya viongozi wote wa Serikali, Dini, chama na wananchi.
Aidha, amesema katika kujenga maendeleo ya Mkoa, hakuna mtu yoyote atakaeonewa kwa namna yoyote ile bali viongozi watafuata Sheria na haki.
Vilevile amewaomba Viongozi wa Dini kutumia nyumba za ibada kuhamasisha maendeleo, kwa watu kufanya kazi kwa bidii badala ya kukesha wakisali pekee.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Zeloth Steven amewataka wananchi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa viongozi wote wa Mkoa ili kuleta maendeleo ya pamoja.
Amesema chama chake kipo tayari kutoa ushirikiano kwa viongozi wote ili ilani ya chama Cha Mapinduzi iweze kutekelezeka kwani wananchi ndio wanachotaka kuona.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Sophia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwala wamesema wapo tayari kutoa ushirikiano kwa viongozi na wananchi wote ili kuleta maendeleo ya Mkoa.
Wakuu wa Wilaya walioteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Juni 19,2021 kwa Mkoa wa Arusha ni Mhe. Sophia Mjema Arusha, Mhe. Eng. Richard Ruyongo Arumeru, Mhe.Raymond Mangwala Ngorongoro,Mhe. Frank Mwaisumbe Monduli na Mhe.a Abbas Kayanda Karatu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa