WANAFUNZI VIONGOZI WA KLABU ZA WATOTO MKOA WA ARUSHA WATEMBELEA BUNGE KUJIFUNZA.
Viongozi wa klabu na mabaraza ya watoto kutoka Halmashauri tatu za Mkoa wa Arusha, Meru, Karatu na Jiji wakiambatana na viongozi toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wataalamu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri pamoja na Viongozi na watumishi toka Shirika la SOS CHILDREN'S VILLAGE wamepata fursa ya kufuatilia shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 13/06/2023 ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo ya siku tano jijini Dodoma.
Viongozi hao wa klabu za Watoto wameshuhudia namna muhimili wa Bunge unavyoendesha shughuli zake ambapo pia watapata fursa ya kutembelea chuo cha Dodoma, Mji wa serikali mtumba na kushiriki maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo inahitimishwa Kitaifa Mkoani Dodoma tarehe 16/06/2023.
Hilda Mgomapayo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, ambaye ni mratibu wa dawati la ulinzi, usalama na maendeleo ya mtoto amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI inasimamia na kuratibu uundwaji wa Klabu hizi ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Mtoto,Sheria za Nchi na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa.
Ikumbukwe shirika la SOS CHILDREN'S VILLAGE Kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mkoa wa Arusha na Halmashauri waliwezesha kuundwa Kwa klabu za watoto mashuleni ambazo zimekuwa msaada na jukwaa muhimu la kuwasilikiliza watoto lakini pia kupokea changamoto zao na kuzifanyia kazi.
Awali akizungumzia umuhimu wa ziara hiyo , Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Arusha ndugu Denis Mgiye amesema Watoto watapata uzoefu na kuongezewa ujasiri wa namna ya kuendesha vikao vyao na kuibua masuala mbali mbali yanayohusu ulinzi na usalama wa Mtoto.
Naye, Afisa Maendeleo ya jamii anayeratibu na kusimamia uundwaji na uendeshaji wa klabu za watoto Mkoa wa Arusha
Bi.Erena Materu amehimiza uundaji wa klabu hizo katika shule zote na ngazi ya jamii kunawasaidia watoto kujisemea na kuomba ushirikiano zaidi,kupewe umuhimu kutoka Idara za kisekta na wadau mbali mbali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa