Wadau wa Maendeleo Mkoa wa Arusha, wamesisitizwa kuweka wazi taarifa za fedha zinazotumika katika kutekeleza shughuli za maendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yote ya mkoa wa Arusha.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha na Mwenyekiti wa Kikao, Missaile Albano Musa, wakati wa kikao cha Kamati ya Lishe Mkoa cha mwezi Januari -Juni, 2024, kilichofanyika kwenye Ofisi ya Katibu Tawala huyo, Agosti 09, 2024.
Missaile amewakumbusha wadau wa maendeleo na Mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya shughuli zao, kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za Serikali, ikiwemo uwazi wa matumizi ya fedha zinazotumika kutekeleza shughuli za kijamii na miradi ya maendeleo.
"Kila ASAS inawajibika kuweka wazi miradi inayotekelezwa na gharama zake kwenye eneo husika, kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa mamlaka za Serikali za Mitaa, hali ambayo licha ya kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wenye tija kwa jamii, zaidi inaiwezesha Serikali kutambua kazi na huduma zinazotolewa kwa wananchi kupitia mashirika hayo yasiyo ya kiserikali". Amesema Missaile
Aidha, amebainisha kuwa, Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, wadau ambao wanaisaidia Serikali, kufika malengo yake ya kuhudumia jamii kisekta pamoja na kusukuma gurudumu la maendeleo la Taifa la Tanzania.
"Tunatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na mashirika ya kiraia, kazi ambayo inatoa mchango mkubwa kwa jamii kwa niaba ya Serikali, mchango ambao wakati mwingine Serikali peke yake isingeweza, hivyo Asas zote za kiraia ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia taratibu na mpango mkakati wa Serikali" Amesema
Kikao hicho cha lishe kinajumuisha wajumbe wa idara mtambuka za Lishe, ikiwemo Elimu,Afya, mipango pamoja na wadau wa lishe kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa