Wananchi wa Mkoa wa Arusha, wamefurahishwa na kuipongeza Serikali ya awamu wa sita kwa kuchagua mkoa huo, kutekelezwa mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu, mradi ambao wanaamini ni fursa kubwa ya kijamii na kiuchumi.
Akitoa salamu za mkoa wa Arusha, kwenye hafla ya Kumkabidhi Mkandarasi eneo la Ujenzi wa uwanja huo wa mpira wa miguu, iliyofanyika kata ya Olmoti, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita, chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuichagua Arusha kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa wawanja wa mpira wa miguu.
"Kwa niaba ya wanaarusha tunaishukuru Serikali chini ya uongozi wa Jemaadari Rais wtu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuichagua Arusha, kujengwa uwanja wa mashindano ya Kimataifa, tunautazamia mradi huu kwa jicho la kipekee licha ya mashindano yaliyoandaliwa kufanyika hapa, tunaiona fursa ya utalii wa michezo Arusha, itakayoendelea kuchochea utalii wa asili uliopo ambao utaendelea kukuza pato la mtu mmoja mmoja, jamii, mkoa na pato la Taifa kwa ujumla.
Aidha ameahidi kutoa ushirikiano wa hatua kwa hatua katika utekelezaji wa mradi huo ikwemo kusimamia upatikanaji wa vibali ili kuhakikisha mradi utakamilika kwa wakati na kufikia malengo ya Serikali na kuahidi kuwa bega kwa bega na Mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Dkt. Damas Damian Ndumbaro amekabidhi kandarasi kwa Mkandarasi wa kampuni ya CRCEG ya nchini China, mradi unaotarajiwa kukamilia mwaka 2026 ukigharimu shilingi Bilioni 286.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa