"Sensa katika Wilaya ya Monduli imesaidia kumuibua mzee wa miaka 120 na sisi kama Wilaya tutajitaidi kuhakikisha wazee kama hawa wanapata mahitaji yao muhimu".
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Frank Mwaisumbe alipokagua zoezi la sensa katika Kijiji cha Arikaria.
Amesema wazee watakaoibuliwa katika zoezi la sensa wao pia watawekewa mazingira rafiki ya kupata huduma zote za kijamii ikiwemo Afya na miundombinu.
Aidha, Mwaisumbe amesema zoezi la sensa kwa siku 2 limeshaweza kubaini mahitaji mbalimbali ya wananchi katika maeneo mengi ikiwemo upungufu wa Maji, vituo vya Afya, miundombinu na shule.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli Rafael Siumbu amesema zoezi la sensa linaendelea vizuri ingawa makarani wanachukua muda mrefu kutoka kaya moja hadi nyingine kutokana na umbali.
Nae, Diwani wa Kata ya Sepeko bwana Diwani Teretui amesema zoezi la sensa katika kata yake litasaidia sana kufahamu kiwango cha huduma mbalimbali za maendeleo kinachoitajika kwa ajili ya wananchi wake.
Mzee mwenye umri wa miaka 120 bwana Masaa Ndale amesema yeye na kaya yake yupo tayari kuhesabiwa kwa manufaa ya vizazi vyake vijavyo.
Zoezi la sensa katika Wilaya ya Monduli linaendelea vizuri katika kata zote na viongozi wa Wilaya wanaendelea kusimamia kwa umakini ili liweze kufanikiwa zaidi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa