Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini tarehe 27.03.2024 ilitoa elimu juu ya madhara ya matumizi na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu kwa Maafisa Udhibiti wapatao 40 wa Mpaka wa OSBP Holili, Wilayani Rombo katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Maafisa waliopatiwa elimu hiyo wanatoka katika Taasisi 20 za Serikali ambazo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Rais, Uhamiaji, Zimamoto, TFS, TMDA, TRA, CED, TAEC, Mifugo, TPHPA, UM, TBS, FISHERIES, CFA, AFYA n. k.
Aidha, Maafisa wa DCEA wa Kanda kwa kushirikiana na Polisi Kata walitoa elimu juu ya madhara ya matumizi na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya hususani Mirungi kwa Madereva Bodaboda na Wabeba Mizigo zaidi ya 50 katika Ofisi ya Kata ya Holili wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.
Baadaye, Maafisa wa DCEA Kanda walimalizia kutoa elimu juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya kwa wanafunzi wapatao 420 wa Shule ya Sekondari Holili mpakani hapo.
Hivyo, elimu hii juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya, udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu pamoja na sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya iliyotolewa itakuwa chachu ya kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya katika mpaka wa OSBP Holili na maeneo ya jirani yanayozunguka katika mpaka huo kwa kuwa wote hao ni wadau muhimu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa